Jumapili 21 Desemba 2025 - 17:00
Wayahudi Waondoke Israel

Hawza/ Rabi wa Kiyahudi, David Feldman, anayehusishwa na shirika la Neturei Karta linalopinga Uzayuni, ameeleza tofauti ya kimsingi kati ya Uyahudi na Uzayuni, na kusisitiza kwamba uhalifu unaotekelezwa dhidi ya Wapalestina hauiwakilishi dini ya Kiyahudi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjama cha Shirika la Habari la Hawza, katika mjadala unaozidi kuongezeka duniani kuhusu kuchanganya Uyahudi kama dini na Uzayuni kama harakati ya kisiasa, na huku dola dhalimu ya Israel ikiendelea kung’ang’ania madai yake na kujitambulisha kama “dola inayowawakilisha Wayahudi”, wakati vita vya mauaji ya kimbari na uvamizi wa ardhi za Palestina vinaendelea, sauti ya Myahudi wa kidini anayepinga simulizi hii inaibuka kwa nguvu.

Rabi wa Kiyahudi, David Feldman, anayehusishwa na shirika la Neturei Karta linalopinga Uzayuni, katika mahojiano maalumu na Arabi 21, alieleza tofauti ya kimsingi kati ya Uyahudi na Uzayuni, na kusisitiza kwamba uhalifu unaotekelezwa dhidi ya Wapalestina hauwakilishi dini ya Kiyahudi, bali unasababisha madhara makubwa kwa Wayahudi duniani kote.

Feldman, katika ujumbe wake wa moja kwa moja kwa vijana wa Kiyahudi walioko ndani ya utawala dhalimu wa Israel, aliwataka waondoke katika dola ya Kiebrania, na akaonya kwamba kuendelea kwa vita vya mauaji ya kimbari hakuwahatarishi Wapalestina na Waislamu pekee, bali pia kunazidisha mara dufu hatari ya chuki na vurugu dhidi ya Wayahudi katika nchi mbalimbali duniani. Pia alieleza mtazamo wake kuhusu suala la suluhu ya dola mbili lililojitokeza hivi karibuni… Na huuuu ndio mkujumuisho wa mazungumzo hayo.

Mwanzoni, tafadhali jitambulishe binafsi na ulitambulishe shirika unalolihusudu.

Jina langu ni Rabi David Feldman, nami nipo katika shirika la kimataifa la Neturei Karta. Sisi ni shirika la kidini la Kiyahudi la kimataifa, linaloinua sauti ya makundi makubwa ya Wayahudi duniani kote katika kupinga falsafa ya Uzayuni, dola ya Israel, na uhalifu wote unaotekelezwa dhidi ya Palestina.

Mtazamo wako ni upi kuhusu kinachoendelea Palestina?

Kinachoendelea Palestina si tu uhalifu kwa mujibu wa sheria za kimataifa na ukiukaji wa viwango vyote vya haki za binadamu, bali pia, kwa mujibu wa dini ya Kiyahudi, ni uhalifu.

Kuua, kuiba, na kuwadhulumu watu wa taifa zima — mambo haya yote ni kinyume na mafundisho ya Kiyahudi, hususan yanapotendeka Palestina. Hawa ni wale wale watu (Wapalestina) waliotuheshimu na tuliishi chini ya ulinzi wao kwa muda mrefu zaidi, hadi miaka ya 1920, pale Uzayuni ulipoingia katika Ardhi Takatifu.

Kwa hiyo, yanayotokea ni makosa, nasi tunajitahidi kuwasaidia watu wavuke mipaka ya propaganda za Kizayuni na waelewe kwamba kupinga uhalifu huu haimaanishi kwamba wanaoukosoa ni watu wanaochukia Wayahudi au ni wapinzani wa Wayahudi.

Je, Israel inawakilisha Wayahudi wote duniani?

Serikali ya Israel haiwakilishi Wayahudi wote, na kwa hakika haiwakilishi dini ya Kiyahudi. Makundi makubwa ya Wayahudi duniani kote yanapinga uhalifu huu wote, na dini ya Kiyahudi inapinga uhalifu huo. Watu wenye dhamiri zilizo hai, watu waaminifu na wanaopenda haki, wanapaswa kuinua sauti zao wanaposhuhudia mbele ya macho yao mauaji ya kimbari ya miaka miwili ambayo bado hayajasimamishwa.

Je, Wayahudi wanaathiriwa na yale ambayo Israel inafanya Palestina, na vipi?

Kwa bahati mbaya, watu wanauawa, watoto wanakufa kwa njaa, na kwa masikitiko makubwa, hali hii bado inaendelea. Tunapaswa kufanya kila tunachoweza ili kuibadilisha hii hali, kusitisha uvamizi huu na kusimamisha haki kwa watu wa Palestina pamoja na usalama kwa watu wa Kiyahudi, kwa sababu Wayahudi wanakabiliwa na athari, chuki na hatari kutokana na yote yanayotendwa kwa jina lao.

Tunaituhumu harakati ya Uzayuni na dola ya Israel, si tu kwa kutekeleza idadi kubwa ya uhalifu dhidi ya Palestina, bali pia kwa kuwaweka watu wa Kiyahudi katika hatari, huku ikisisitiza kufanya uhalifu wake wote kwa jina la jamii nzima ya Kiyahudi.

Tofauti kati ya Uzayuni kama itikadi na Uyahudi ni ipi?

Ni muhimu sana kuelewa tofauti kubwa kati ya Uyahudi na Uzayuni. Uyahudi ni dini. Kila kitu kwenye Uyahudi kinajengwa juu ya imani kwa Mwenyezi Mungu na utekelezaji wa amri Zake; humo hakuna siasa wala utaifa, na kwa hakika hakuna uhalifu. Ilhali Uzayuni ni harakati ya kisiasa tupu, iliyoanzishwa na watu wasiobeba dhamana ya kufuata sheria za Uyahudi, na wanaoitumia vibaya dini ambayo wao wenyewe wanakataa kuifuata, ili kuhalalisha uhalifu ambao katika dini hiyo ni haramu.

Mnakabilianaje na itikadi hii (Uzayuni) ambayo, kama mlivyosema, inaharibu taswira ya Uyahudi?

Harakati ya Uzayuni, kama nilivyosema, ni hatari kwa ubinadamu na ni kudhalilisha Jina la Mungu. Njia tunayopambana nayo ni kupitia mapambano ya uelimishaji na uhamasishaji. Watu wengi hawana taarifa za msingi kabisa. Vyombo vikuu vya habari haviwawasilishii watu taarifa muhimu sana wanazozihitaji ili kufanya maamuzi sahihi.

Sisi tupo hapa kufundisha, tupo hapa kusambaza uelewa na kueleza kile ambacho Uyahudi unafundisha kuhusu hali hii. Kupitia hilo, tunawasaidia watu kuachana na propaganda, kuelewa kinachoendelea, na kutambua kwamba kuwa mwema na mwenye haki hamaanishi kuwa mtu wa kuwachukia Wayahudi. Watu hawapaswi kuogopa kuinua sauti zao dhidi ya dhulma hii.

Je, mnayoyazungumza yanafanana na kinachoendelea ndani ya Israel kisiasa kuhusu kuandikishwa kwa Wayahudi wa kidini katika jeshi?

Ndiyo. Vijana hao katika Ardhi Takatifu wanaokataa kuhudumia jeshi la Israel hawaamini katika dola ya Israel. Wanapambana na kufanya kila wawezalo ili wasifanye uhalifu huo kwa mikono yao, wala kushiriki kwa vitendo katika uasi dhidi ya Mungu kwa kuunga mkono uhalifu huo.

Kwa bahati mbaya, wavulana na wasichana hawa, wanapofikisha umri wa miaka kumi na saba, wanahesabiwa moja kwa moja kuwa wahalifu, kwa sababu tu hawahudumii jeshi. Nina rafiki yangu aliyeikimbia serikali ya Israel na hataki tena kuishi chini ya mfumo huu, lakini watoto wake wawili hawawezi kuondoka nchini, kwa sababu wakifika uwanja wa ndege watakamatwa.

Unaonaje makabiliano yanayoendelea kati ya Waisraeli na Wapalestina huko Ghaza?

Hali ni mbaya sana. Tunaamini kwamba yanayotokea hayakuanza leo, wala jana, wala miaka miwili iliyopita, wala hata miaka kumi na sita iliyopita ilipoanza mizingiro. Yalianza miaka 77 iliyopita, au hata kabla ya hapo, pale harakati za Kizayuni zilipoanza takribani miaka 100 iliyopita. Kama nilivyosema, huu ni mzunguko usio na mwisho. Kwa masikitiko makubwa, maadamu hatutashughulikia chanzo kikuu, ambacho ni uvamizi, sioni mwisho wake.

Ujumbe wako kwa vijana walioko ndani ya Israel ni upi? Unawaambia nini?

Ninachowaambia watu walioko Israel ni kwamba; ni wakati wa kuamka na kuelewa kwamba kuna jambo lisilo sawa. Tunapaswa kuelewa kwamba ahadi ambazo harakati ya Uzayuni ilitupa—usalama huu, ulinzi huu, na taifa hili kwa Wayahudi—kimsingi zilikuwa za uongo na tangia mwanzo zilipingana na misingi ya imani ya Kiyahudi.

Hata kama baadhi hawakutambua hilo mwanzoni, angalau sasa tunapaswa kuelewa kwamba hili halina manufaa kwa yeyote. Kwa bahati mbaya, uhalifu mwingi unatendeka, dhulma kubwa ipo, na hatari kubwa inazikabili pande zote.

Ni lazima tuache kuunga mkono harakati ya Uzayuni, maadamu mfumo wa Kizayuni upo, kila mtu yuko hatarini, wakiwemo Wayahudi.

Ninamhimiza kila Myahudi, mwanamke na mwanaume, kuondoka nchini, kwa sababu maisha yao yako hatarini, hali yao ya kisaikolojia iko hatarini, na Uyahudi wao uko hatarini. Pale ni mahali pa hatari, nasi tunawahimiza watu waache propaganda za Kizayuni, waache Uzayuni, waache dola ya Israel, na warejee katika historia ya kale kabla ya Uzayuni.

Je, unaunga mkono kanuni ya suluhu ya dola mbili?

Hapana. Nakubali ile sehemu inayorejeshwa kwa Wapalestina, lakini sikubaliani na ile inayobaki mikononi mwa mashirika ya Kizayuni, kwa sababu hilo kwa mujibu wa Uyahudi ni kosa, na kivitendo halileti haki tunayoihitaji hapa. Tunachosema ni kwamba lazima uvamizi huu wa Kizayuni Palestina ukomeshwe kabisa, haki zote zirejeshwe kwa wote waliodhulumiwa, wakimbizi wote waruhusiwe kurejea, na wakaazi halisi wa Palestina waruhusiwe kuchagua serikali yao.

Taswira yako ni ipi kuhusu ardhi ambayo Wayahudi wanaishi—chini ya dola ya Palestina au chini ya dola ya Kiyahudi ya Israel?

Ni lazima tutumie historia ya nyuma kujibu swali hili. Tayari tumeona kilichotokea chini ya dola ya Kiyahudi: ni ukiukaji wa dini ya Kiyahudi na hauleti amani. Lakini uwepo wa dola ya Palestina, uwepo wa utawala wa Kiislamu katika ardhi hii, tayari tumeuona hapo awali na ulikuwa na mafanikio kamili. Hivyo ndivyo ilivyokuwa zaidi ya miaka 100 iliyopita, na hilo ndilo tunalopaswa sote kulitazamia katika siku zijazo.

Watu wenye mtazamo kama wetu katika Ardhi Takatifu wanasema wanataka dola isiyo ya Kiyahudi katika Ardhi Takatifu, na wanasema haijalishi dola ambayo Wapalestina wataichagua itakuwa ipi—hata kama itakuwa dola ya Kiislamu—bado itakuwa bora zaidi kuliko hali ya leo. Dola ya Kiislamu itawalinda Wayahudi zaidi kuliko ilivyo leo na itaiheshimu dini ya Kiyahudi.

Mwisho, mtazamo wako ni upi kuhusu hatua za baadhi ya serikali za Kiarabu katika kuhalalisha uhusiano na Israel, na hatua za jumla za Marekani katika kuiunga mkono Israel?

Mimi ni Myahudi, na naweza kutoa mtazamo wa Myahudi wa kidini kuhusu yote yanayoendelea. Inasikitisha sana na inatia wasiwasi mkubwa kuona wakati mwingine uungaji mkono wa kipofu kwa Israel, ilhali hili, kwa bahati mbaya, ni uasi dhidi ya Mungu na ni uharibifu wa ubinadamu, na linawaathiri wote wanaohusika nalo. Tunatumaini na tunawaomba wanasiasa waache propaganda, watafakari upya mahusiano yao na Israel, na wasimame upande wa ubinadamu.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha